Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, Mari al-Ali, mwanaharakati wa kitamaduni kutoka Syria, katika kikao maalumu cha “Hija; Mahali pa Miadi ya Umoja” kilichofanyika leo Jumatano kwa juhudi za Majma' al-'Alami li-Taqrib al-Madhahib al-Islamiyyah, alisema kwamba; Hija ni moja ya maonesho makubwa zaidi ya kibinadamu na kiroho ambapo umoja na mshikamano wa Waislamu hudhihirika, na akaongeza: Faradhi hii si ibada ya kidini pekee ambayo Muislamu huitekeleza mara moja katika maisha yake, bali ni kongamano la kimataifa la kila mwaka ambalo mamilioni ya nyoyo kutoka katika jamii, lugha na tamaduni mbalimbali hukusanyika chini ya bendera moja na kwa kauli mbiu moja: “Labbayka Allahumma Labbayk.”
Aliendelea kusema: Katika zama ambazo kampeni za chuki dhidi ya Uislamu zimeundwa na chuki dhidi ya Uislamu inaendelea kuongezeka katika baadhi ya jamii za Magharibi na vyombo vya habari, Hija imejitokeza kama ujumbe wa kiistaarabu na kibinadamu unaosisitiza kwamba Uislamu ni dini ya umoja, amani na maelewano kati ya mataifa.
Mwanaharakati huyu wa kitamaduni wa Kisyria alikumbusha kwamba; takwimu rasmi zilizotolewa na “Shirika la Takwimu za Umma la Saudi Arabia” zinaonesha kuwa, idadi ya mahujaji katika misimu ya hivi karibuni imevuka watu milioni moja na nusu kwa mwaka; mahujaji wanaotoka katika nchi kadhaa duniani na ambao kila mwaka huumba mandhari za kipekee zinazoonesha uwezo wa Uislamu wa kuwakusanya wafuasi wake bila kujali tofauti za kitaifa na mahusiano ya kitamaduni. Mkusanyiko huu mkubwa wa kibinadamu hauna mfano katika tukio lolote jingine la kimataifa, kwa sababu Waislamu hukusanyika humo kwa msingi wa aqida na maadili ya pamoja, bila ya kuzingatia tofauti za kikabila, kitaifa au kitabaka.
Al-Ali alikumbusha kuwa: Miongoni mwa maana kuu za Hija ni kuondoa tofauti kati ya wanadamu; humo hakuna tofauti kati ya tajiri na maskini, Mwarabu na asiye Mwarabu, mweupe na mweusi. Wote huvaa Ihramu kwa namna moja, hutekeleza ibada kwa namna moja na husimama katika sehemu moja; huu ni uthibitisho wa kivitendo wa msingi wa usawa wa kibinadamu ambao Uislamu ulitangaza zaidi ya karne kumi na nne zilizopita, taswira hii ya kimataifa inayojirudia kila mwaka inabatilisha madai mengi yanayojaribu kuonesha kwamba Uislamu ni dini iliyofungwa, yenye ubaguzi na inayotegemea migongano ya kiustaarabu.
Akiashiria kauli ya Ali Shariati, aliongeza kusema: Katika kitabu chake mashuhuri “Hajj (Faradhi ya Tano)” alitoa mtazamo wa kina kuhusu Hija. Aliamini kwamba Hija si mkusanyiko wa ibada tu, bali ni “maonesho ya umoja” na “kongamano la kimataifa la umma wa Kiislamu”, Al-Kaaba ni alama ya kitovu cha umoja wa kiroho wa Waislamu wote, na kufanya Twawafu ni alama ya umoja wa lengo na hatima yao ya pamoja, wakati Ihramu nayo inadhihirisha hali ya kujivua tofauti za kijamii na kimada ili mwanadamu arudi katika hakika yake safi ya kibinadamu.
Al-Ali alisisitiza kuwa: Hija si safari ya kiroho pekee, bali ni tajriba ya utambuzi wa kiustaarabu na kijamii ambayo ndani yake Muislamu huhisi kuwa yeye ni sehemu ya umma mkubwa unaovuka mipaka, jiografia na lugha. Kutokana na hilo, ujumbe wa kitamaduni na kibinadamu wa Hija hudhihirika; kwa sababu huwasilisha kwenye ulimwengu taswira halisi ya Uislamu kama dini iliyojaa umoja, uadilifu na uvumilivu, na hushinda juhudi za kuchafua sura ya Waislamu na kuwaonesha kama jamii zilizotawanyika au zinazopigana wao kwa wao.
Maoni yako